Mjumbe wa Bunge la Kaunti ya Kitui anayewakilisha Wadi ya Yatta Kwa Vonza, Mheshimiwa Mark Ndingo, amejiunga na viongozi wengine nchini kuomboleza kifo cha Waziri Mkuu wa zamani, Rt. Hon. Raila Amolo Odinga, ambaye amefariki dunia nchini India akiwa na umri wa miaka 80, kwa mujibu wa taarifa za familia.
Katika ujumbe wake wa rambirambi, Mheshimiwa Ndingo alielezea huzuni kubwa kufuatia kifo hicho, akimtaja marehemu Raila kama kiongozi shujaa na mtetezi wa haki za binadamu ambaye mchango wake umeacha alama isiyofutika katika siasa za Kenya.
“Tumesikitishwa sana na kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Mheshimiwa Raila Odinga. Tumepokea habari hizi asubuhi, na ni pigo kubwa sana kwa familia yake na taifa kwa jumla — si Kenya pekee bali hata bara zima la Afrika,” alisema Mheshimiwa Ndingo.
Aidha, alimsifu marehemu Raila kwa moyo wake wa uzalendo na mapambano yake kwa ajili ya umoja wa taifa na uongozi wa haki.
“Raila amekuwa akipigania haki za binadamu kwa muda mrefu. Alikuwa mtu aliyependa kuona nchi ikiwa na umoja na hakuwa na woga kusema ukweli kuhusu makosa ya serikali. Ni pigo kubwa sana kwetu sote. Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi,” aliongeza.
Kenya kwa sasa inaendelea kuomboleza kifo cha Raila Odinga, kiongozi ambaye urithi wake katika safari ya demokrasia na umoja wa taifa utadumu milele.