Rais William Samoei Ruto ameendeleza mashambulizi yake ya kisiasa dhidi ya viongozi wa upinzani, akiwakejeli kwa madai kwamba hawana ajenda ya kujenga taifa, bali kazi yao ni kufanya maandamano na kurudia misemo ya “Onetam, Kasongo, Must Go”.
Akihutubia wananchi katika ziara yake ya maendeleo sehemu za Ukambani, Rais Ruto alisema baadhi ya wanasiasa wa upinzani wamefeli kutoa suluhu kwa changamoto zinazowakabili Wakenya, na badala yake wamegeukia siasa za porojo zisizo na tija.
“Hawa watu kazi yao ni kusema ‘Onetam, Must Go, Kasongo’, lakini hawawezi hata kueleza mpango wa kuleta unga chini au kuongeza ajira kwa vijana. Sisi tunafanya kazi, wao wanapiga kelele,” alisema Rais Ruto huku umati ukishangilia.
Ruto alisisitiza kuwa serikali yake inaendelea kutekeleza miradi mikubwa ya maendeleo kwenye sekta ya barabara, kilimo, maji na elimu, akitaja kuwa wananchi watapima viongozi kwa kazi, si maneno matupu.
Aidha, alitaka viongozi wa upinzani kujipanga na kutoa sera mwanana kama wana nia ya kuongoza taifa badala ya kulalamika kila siku.
“Ukisema lazima mtu aondoke, unakuja na nani? Na sera yako ni gani? Hiyo ndio Wakenya wanataka kusikia, sio makelele kila siku,” aliongeza.
Kauli ya Rais imeibua mjadala mkali katika medani za siasa, huku wandani wa upinzani wakimshutumu kwa kukosa kujibu matatizo halisi kama bei ya vyakula, ushuru na gharama ya maisha.
Hata hivyo, Rais Ruto amesisitiza kuwa serikali haitatetemeshwa na kauli za upinzani, akisema “maendeleo ndiyo itakuwa jawabu la kelele zao zote.”

Kwa taarifa zaidi, tembelea www.thecountydiary.co.ke
